Monday, September 19, 2011

CCM yaishambulia Igunga kama nyuki Daniel Mjema, Igunga
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeanza kulishambulia jimbo hilo kwa mikutano ya hadhara na sasa kwa siku kinafanya mikutano zaidi ya 40 na kimeongeza kikosi kingine kinachomhusisha Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Philip Mangula.

Awali, CCM ilikuwa na kampeni za timu mbili zilizokuwa zikifanya wastani wa mikutano nane kwa siku lakini kuanzia jana timu hizo za kampeni zimegawanywa katika makundi 12 yanayowahusisha viongozi wa kitaifa.

Katika mpango huo wa kushambulia jimbo hilo la Igunga, kila kundi linafanya mikutano minne ya hadhara kwa siku ambayo kwa hesabu rahisi ni kwamba, kila siku inafanyika jumla ya mikutano 48.

Viongozi wanaounda timu hizo ni pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, Mangula, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai na baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu(NEC).

Wajumbe hao ni pamoja na makatibu wa kuu wa jumuiya za chama hicho ambao ni Martin Shigella wa Umoja wa Vijana( UVCCM), Amina Makilagi wa Umoja wa Wanawake(UWT) na Hamis Dadi, Umoja wa Wazazi.

Kikosi hicho kimeongezewa nguvu na Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha na Mratibu wa kampeni za CCM Igunga, Mwigulu Nchemba, Katibu wa NEC Oganaizesheni, Asha Abdalah Juma na Katibu wa CCM Ilemela, Shaibu Akwilombe.

Kabla ya kujiunga CCM, Akwilombe aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na anatumika kama mhamasishaji dhidi ya Chadema, kwani hata alipoondoka chama hicho alikishutumu kwa mambo mbalimbali ikiwamo ubinafsi na siasa za ukabila.

CCM katika kuweka ngome yake imara jimboni humo, pia imemwongeza katika Mjumbe wa NEC na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde na wajumbe wa sekretarieti ya Kamati Kuu ya CCM ambayo ilitarajiwa kufanya kikao chake jana katika jimbo hilo.

Lusinde atema cheche
Akihutubia moja ya mikutano ya hadhara katika kijiji cha Majengo kata ya Chabutwa jana, Lusinde aliwataka wananchi wamchagua mgombea wa CCM, Dk Dalaly Kafumu, kwa kuwa ndiye mwenye uwezo wa kutatua kero zao.

“Jino lililong’oka ni la CCM, hivyo rudisha tena jino la CCM… Hebu niwaulize, kama ikitokea bahati mbaya Sheikh wa msikiti amefariki dunia mnaweza kumleta mchungaji atoe huduma msikitini?” alihoji Lusinde.

Akizungumzia kile alichodai wafuasi wa CCM kufanyiwa vurugu na makada wa Chadema, Lusinde alisema vijana wa CCM sio kwamba, hawawezi ugomvi bali hawataki ugomvi na wanaamini utawala wa sheria.

"Tunataka tushindane kwa hoja sio ugomvi na upole wetu wasifikiri kuwa hatuuwezi ugomvi... tukiamua kujibu mapigo hapa hapatakalika tunaomba nao wawe wastaarabu," alitahadharisha Lusinde.

Dk Kafumu ajiita mwadilifu
Kwa upande wake, Dk Kafumu aliwaomba wananchi hao wamchague kuwa mbunge wao kwa kuwa ni mwadilifu na kukanusha tuhuma kuwa ameshiriki kuliingiza taifa katika mikataba mibovu ya madini.

Wakati huohuo, vijana wanaodhaniwa ni wafuasi wa Chadema, jana walilirushia mawe gari lililokuwa likitumiwa na Lusinde katika msafara wa kuelekea katika mkutano wa hadhara wa kampeni kijiji cha Majengo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Lusinde alisema tukio hilo lilitokea jana saa 5:00, asubuhi katika kata ya Nkinga Kati ambapo jiwe hilo liliharibu kioo cha nyuma cha gari aina ya Toyota Prado T888 ALL.

Lusinde alisema wakati wakipita barabarani, walitokea vijana wakiwa chini ya mti uliotundikwa bendera ya Chadema katika eneo hilo la Nkinga Kati na kurusha mawe kuelekea kwenye gari lao na kuharibu kioo hicho.
Tukio hilo la kushambuliwa Lusinde ni mfululizo wa matukio ya siasa za hatari yanayofanywa na watu wanaodhaniwa ni wafuasi wa Chadema ikiwamo tukio la kumvamia Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.

No comments: