Rais Jakaya Kikwete akiwa Zanzibar kutoa pole kwa wafiwa na
Mmoja wa waokoaji akijifuta machozi wakati akipeleka nchi kavu moja za maiti za watoto waliokufa katika ajali ya meli katika pwani ya Nungwi Zanzibar
Umati wa wakaazi wa Zanzibar wakiwa bandarini
Sehemu ya walionusurika katika ajali hiyo
Wazamiaji shupavu wakiwa na mmoja wa watoto waliookolewa
Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad na Rais Mstaafu wa Zanzibar Mh Amani Abeid Karume na viongozi wengine wakiwa mstari wa mbele kutembelea kambi ya waliopatwa na ajali uwanja wa Maisara
Rais Dkt. Jakaya Kikwete akiwa ameongozana na mke wake Mama Salma Kikwete akitoa pole kwa wafiwa mara baada ya kuwasili uwanja wa Maisara
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jioni ya leo, Jumamosi, Septemba 10, 2011, ametembelea Viwanja vya Maisara mjini Zanzibar kujionea mwenyewe zoezi la kutambua miili iliyoopolewa kutoka baharini kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya Mv Spice Islander alfajiri ya kuamkia leo.
Akifuatana na Mama Salma Kikwete, Mheshimiwa Rais Kikwete amewasili Uwanja wa Ndege wa Zanzibar saa 12:10 jioni na kwenda moja kwa moja kwenye Viwanja vya Maisara ambako mamia kwa mamia ya waombolezaji walikuwa wamekusanyika kujaribu kutambua miili za jamaa, ndugu na wapendwa wao ambao wamepoteza maisha katika ajali hiyo.
Kwenye Viwanja hivyo, Rais Kikwete amepokelewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (SMZ) Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wawili wa Rais wa Zanzibar, Waheshimiwa Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Idd, Rais Mstaafu wa Zanzibar Mheshimiwa Amani Abeid Karume na uongozi karibu wote wa juu wa SMZ.
Hali ilikuwa ya huzuni sana kwenye Viwanja hivyo wakati Mheshimiwa Rais akifuatana na uongozi huo wa juu wa Zanzibar ulivyopitia kwenye mahema ya muda ya zoezi ya utambuzi wa miili ya watu waliopoteza maisha yao katika ajali hiyo ya meli hiyo iliyokuwa inasafiri kutoka Dar-Zanzibar-Pemba. Imezama katika eneo la Nungwi, Zanzibar.
Katika eneo hilo la utambuzi, Mheshimiwa Rais ameshuhudia miili ya watu wazima iliyokuwa imefungwa ama kufunikwa na ile ya watoto wadogo ambao sura zao zilikuwa zimeachwa wazi kwa ajili ya utambuzi wa haraka kwa mujibu wa sura zao.
Kwenye Viwanja hivyo, Mheshimiwa Rais ameambiwa kuwa hadi jioni hiyo ya leo, watu kiasi cha 192 walikuwa wamethibitishwa kuwa wamepoteza maisha na miili yao kuopolewa wakati kiasi cha watu 630 walikuwa wameokolewa kutoka ajali hiyo ya meli ambayo hadi sasa haijulikani ilikuwa imebeba watu wangapi.
Baadaye, Rais Kikwete ametembelea Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwaona na kuwatakia heri waliokoka katika ajali hiyo na kulazwa katika hospitali hiyo ya Serikali.
Hadi jioni ya leo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilikuwa imechukua maamuzi kadhaa kukabiliana na hali ya ukoaji wa watu katika ajali hiyo. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuchangia kiasi cha sh milioni 300 ili kusaidia zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kusaidia kusafirisha na kuzika miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo. SMZ imetoa sh milioni 100 kwa shughuli hiyo.
Serikali ya Muungano pia imeamua kukubali msaada wa wapigaji mbizi kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya kusaidia kufanya tathmini ya jinsi meli ilivyozama na kuokoa maisha ya watu ambao watakuwa wamebanwa ndani ya meli hiyo.
Kesho, Jumapili, Septemba 11, 2011, Kamati ya Taifa ya Ulinzi na Usalama itafanya kikao chake mjini Zanzibar kuzungumzia hali ya ajali hiyo kwa maana ya kupata maelekezo kamili kuhusu ajali hiyo, kupokea ripoti ya ajali, kufanya tathmini ya ripoti hiyo na kutoa maelekezo ya jinsi ya kukabiliana na hali ya sasa na hali ya baadaye ya usafiri wa maji nchini.
Hata kabla ya kikao hicho, tayari Mheshimiwa Rais Kikwete ameamua kufanyika kwa uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment